Je wewe ni mtu wa kupenda ghafla, yaani mwanaume anapokutamkia kwamba
anakupenda huwa unamuamini kwa kiasi gani, unakuwa ni mwepesi wa
kumuamini na kujitoa kwa ajili yake au unakuwa na kujivuta vuta ili
kujiridhisha kabla ya kuingia katika uhusiano? Hebu fikiri kabla ya
kuamua, jipe muda kwani hakuna jambo
lililo jema kama subira linapokuja swala la kupenda. Subira itakuepusha
kupoteza muda wako katika mahusiano ambayo hayana mashiko wakati
dhamira yako ilikuwa ni kumpata mwenzi mwenye sifa muafaka, pale
utakapoingia mahali ambapo sipo. Kwa kawaida kutoka katika uhusiano huo
kuna gharama kubwa na kunaweza kukusababishia matatizo mengi yakiwemo ya
kiafya. Hapa chini nitajaribu kueleza makosa kadhaa ambayo wanayafanya wanawake linapokuja swal la kupenda:
1.Kumbadili mtu awe vile utakavyo:
Usije ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha mtu mzima na akili zake.
Kama umepata mwanaume ambaye kwa mtazamo wako unamuona ana sifa muafaka
lakini anatabia ambazo huzipendi kwa mfano ulevi au kuvuta sigara vitu
ambavyo vinakukera sana, usije ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha
na akaacha tabia hizo, anaweza kuacha kwa muda tu ili kukuvuta ukiingia
kingi imekula kwako, tabia hiyo inaweza kujirudia. Ni vyema kama kuna
tabia ambazo umezipenda lakini zipo ambazo huzipendi kutoka kwa mwenzi
wako, basi weka uzingativu kwenye zile tabia unazozipendfa na zile
usizozipenda achana nazo, kama ataamua mwenyewe kuziacha sawa lakini
kama akiamua kuendelea nazo, basi zisikuumize kwani unaweza kujikuta
ndoa yako inakuwa na migogoro isiyokwisha kwa sababu ya kuonekana una
ghubu kwa kujaribu kumbadilisha mwenzi wako na mwisho wake upendo
unakuwa haupo na kisirani katika ndoa kinaongezeka. Kitendo cha
kuonekana kuwa na ghubu kinaweza kumuingiza mwanaume katika tabia
nyingine mbaya ya kutotumia muda mwingi kukaa nyumbani kwake na kutafuta
kampani nyingine, kama akipata kampani ambayo siyo nzuri anaweza
kuangikia katika nyumba ndogo ambayo itamkubali bila masharti.
2.Njoo tuishi:
Unaweza kukutana na mwanaume ambaye ana nyumba nzuri au amepanga nyumba
nzuri na ana kila kitu ndani pamoja na usafiri, anakuwa mwepesi kukupa
funguo za nyumba yake ili uhamie muishi pamoja, lakini haweki msimamo
wake wazi kwamba ana matarajio gani na wewe. Kabla ya kukubali kupokea
funguo na kuhamia kwake jiulize kama unampenda kwa dhati au umekubali
kwa sababu ya nyumba yake nzuri. Kumbuka nyumba na vitu vingine
vinavyotizamika kwa macho (material things) havina mashiko linapokuja
swala la kupenda. Kupenda kunahusisha vitu vya ndani kama vile kupenda
kwa dhati bila masharti wala kuangalia sifa za nje, kuwa na amani moyoni
kila umwonapo mpenzi wako, kuwa na furaha wakati wote mnapokuwa pamoja,
kupatwa na msisimko wa mapenzi
kila umwonapo au usikiapo sauti yake nk. Lakini kama utamkubali
mwanaume kirahisi kwa sababu tu kakukabidhi funguo za nyumba yake wakati
huna mapenzi ya dhati ni janga kubwa kwa sababu hivi vitu vya nje
vinaweza kutoweka kirahisi, sasa je ikitokea si mapenzi nayo yatakuwa
yamekwisha? Kumbuka kwamba kile kilichokupeleka kwake hakipo.
3.Amekuwa ni liwazo kwako
Liwazo linaweza kuwa sehemu ya
mapenzi lakini hivi vitu haviendi pamoja. Unaweza kuwa na mwanaume
ambaye mnapendana na mnakamilishana hii ni tofauti na mwanaume
unayempenda na ukamgeuza kuwa liwazo pale unapohisi upweke. Jiulize, je
ni kwamba mnapendana na mnafurahi kuwa pamoja au unampenda kiasi kwamba
huwezi kuishi bila uwepo wake. Hapa nazungumzia utegemezi wa kihisia,
yaani unakuwa king’ang’anizi
mpaka mwanaume anakuona kero, badala ya kufurahia mahusiano yenu
mwanaume anakuona kuwa ni kero kutokana na kuwa tegemezi wa kihisia.
Hakuna mwanaume anayependa mahusiano ya aina hii anachoka haraka kihisia
na atajitahidi kwa kila namna kukukwepa na ikiwezekana kukutosa na
kutafuta ustaarabu mwingine jambo ambalo litakuumiza sana.
4.Mwanaume king’ang’anizi:
Mwanaume kutongoza na kukataliwa siyo jambo linalowashughulisha sana kwao kujaribu na kukosa ni sehemu ya maisha, lakini lipo
suala la kung’ang’ania, yaani mwanaume kumfuatilia mwanamke kwa hali na
mali na kujitoa ili kuhakikisha anampata mwanamke anayemtaka. Huu ni
mtego wa mapenzi, kwani kwa mwanaume kung’ang’ania na kufuatilia
mwanamke kwa muda mrefu bila kuchoka hata asumbuliwe kiasi gani
haimaanishi kwamba mwanaume huyo amempenda mwanamke huyo. Wakati
mwingine ni matamanio tu ndiyo yamemsukuma kutokana na sifa za nje alizo
nazo mwanamke huyo. Kupenda kwa mwanaume kunahusisha zaidi sifa za nje
kuliko za ndani na ndiyo maana mapenzi ya aina hiyo hayadumu yanaanza
kama kichaa na kuyeyuka ghafla kama kipande cha barafu juani. Pale
mwanamke anapokutana na mwanaume king’ang’anizi na asiyekubali jibu la
hapana, kabla ya kukubali ajiulize kama anakubali kuwa na mahusiano na
mwanaume huyo kwa sababu amempenda kwa dhati au kwa sababu ya
uking’anga’nizi wake? Kumbuka kwamba wapo baadhi ya wanawake wanaweza
kumkubali mwanaume tu kwa sababu amemfuatilia sana, anajiwa na huruma
anakubali kuwa na mausiano naye siyo kwa sababu amempenda bali kwa
sababu ya huruma. Ni vyema ukajiuliza kama na yeye atathamini huruma
yako au akishapata alichokitaka atakugeuka na kuwa mwiba mchungu kwako?
Tafakari na chukua hatua.
5.Baada ya kupanda mbegu mmea ukachipua
Umekuwa na uhusiano na mwanaume huyu kwa muda mrefu, lakini hakuwahi
kukutamkia kwamba ana matarajio gani na wewe kuhusiana na swala la ndao,
ghafla unakoma kuziona siku zako… Mimba hiyo! Je unafanyaje?
Kwanza naomba ufahamu kwamba, kupata mimba haimaanishi ndiyo kuolewa.
Hili ni kosa ambalo wanalifanya wanawake wengi tena wa kiwango cha
kutosha, wanaamini kwamba kubeba mimba kutawahakikishia kuolewa na
mwanaume aliyempa ujauzito. Kwa huku kwetu sheria haziwabani sana
wanaume linapokuja swal la kulea mimba na matunzo ya mtoto kwa hiyo
mwanaume kumtosa mwanamke aliyebeba ujauzito siyo jambo la kushangaza.
Wanawake ambao ni single mother
wanajua kuhusu jambo hilo. Kwa hiyo kama unabeba mimba fanya hivyo
ukiwa umejiandaa kujitwika changamoto zitakazojitokeza na usije
ukajifariji ukidhani kutakuwa na masaada kutoka kwa mwenzi wako, utakuwa
unajidanganya. Kama akikubali mfunge ndoa sawa, kama akikubali kulea
mimba na mtoto atakeyezaliwa pia ni sawa, akikataa wala usivunjike moyo,
simama imara na songa mbele na maisha kwani kuzaa kabla ya ndao siyo
mwisho wa maisha, yapo maisha tena mazuri sana ukiwa na mwanao. Kwanza
unaye mtu wa kukuliwaza, na pili utakuwa umajihakikishia kwamba wewe si
mgumba, na tatu leo na kesho umekuwa mtu mzima unaye wa kukushika bega
kuliko kutegemea ndugu zako.
6.Pesa inapokuwa sehemu katika kupenda.
Wapo baadhi ya wanawake kabla ya kumkubalia mwanaume wanaangalia
anamiliki kitu gani, amesoma kwa kiwango gani, ana kazi ya aina gani,
anafanya shughuli gani, anazo fedha za kutosha au yuko katika mazingira
ya utafutaji yanayoashiria neema huko mbeleni. Sikatai kwamba wanawake
kabla ya kumkubali mwanaume wanataka kujihakikishia usalama, na kama
nilivyowahi kusema hapa mara
nyingi kwamba usalama kwa mwanamke maana yake ni mtu kuwa na fedha,
tofauti na zama za kale za mawe ambapo uwindaji na kilimo kilimuweka
mwanaume shupavu katika nyanja hizo kukimbiliwa na wanawake. Siku hizi
hayo hayapo, fedha imekuwa ni njia ya mkato katika kupata kila kitu. Kwa
mwanamke fedha ni mtego umnasao kama panya na kipande cha nguru
mtegoni. Siku hizi ukiwa na fedha una uwezo wa kumpata mwanamke
umtakaye, fedha imekuwa kama tufani, inabeba waliomo na wasiokuwemo,
hata wale watakaotokwa na povu kupinga hoja hii, nadhani hawajapata
bahati ya kukutana na wanaume wenye fedha, laiti wangepata wasingeweza
kusimama hapa na kupinga hoja hii. Kwa ushauri tu, si vibaya kuangalia
mwanaume mwenye muelekeo wa kutafuta lakini hicho kisiwe ni kigezo namba
moja, kwani kama akikuonyesha sifa hizo kabla ya kuingia kwenye
uhusiano kisha ukaingia na baadaye ukagundua mwanaume huyo si mali kitu
wenyewe mnaita mwanaume suruale, utaumia sana.
7. Uzuri wa kitandani
Ninaposema uzuri wa kitandani namaanisha kuridhishana katika tendo la
kujamiiana, kwa kawaida wanawake ndiyo wahanga wakubwa linapokuja swala
la njaa chumbani, wao ndiyo kwa asilimia kubwa hawaridhishwi na wenzi
wao katika tendo. Siyo kwamba waume zao wana udhaifu, la hasha,
inawezekana wanazo nguvu kama za simba, lakini kwa kawaida tendo la
kujamiiana haliwi zuri eti kwa sababu tu mwanaume anazo nguvu kama za
simba, bali inahitaji
usanii na utundu ukiwemo werevu wa kihisia kuweza kumfikisha mwanamke
kileleni. Wanaume wengi kwa sababu ya mazoea wanadhani swala la
kumfikisha mwanamke kileleni ni kutwanga kwa kutumia msuli. Si kweli
hata kidogo, ni kumuandaa mwanamke kwa maneno matamu kabla hata ya
kuelekea kitandani. Kwa hiyo wapo wanaume wenye ufundi huo linapokuja
swala la kujamiiana, nia mafundi hodari wenye uwezo wa kuwafikisha wenzi
wao peponi, lakini inawezekana katika maeneo mengine ya kimaisha wakawa
watupu kabisa. Siyo wawajibikaji, wanyanyasaji wakubwa, hawana staha,
hawawaheshimu wenzi wao na ni wenye vurugu kichwani. Wakati mwingine
mwanamke anaweza kunasa kwa sababu hiyo tu, ya ufundi wa kitandani,
lakini akajikuta anaishi katika machungu kutokana na kutothaminiwa na
kunyanyaswa kupita kiasi. Kinachomuweka si kingine ni ile starehe ya
muda mfupi wawapo kitandani tu basi. Kuna haja ya kujiuliza, Je ni kitu
gani hasa kinachokufanya umpende mwenzi wako? Kama utamkubali na udhaifu
wake na una uwezo wa kuhimili hizo tabia zisizofaa kwa maana kwamba
hazikuumizi kihisia (kitu ambacho si rahisi sana kwa wanawake) ni sawa,
lakini kama huwezi, sikushauri kuingia katika uhusiano wa aina hiyo,
kwani ni kujitafutia kaburi la mapema.
0 comments:
Post a Comment